12 Agosti 2020 - 09:30
Watu 40,000 wakimbia machafuko mapya Kivu Kusini nchini DRC

Watu wasiopungua 40,000 wamekimbia machafuko ya kikabila katika eneo la milimani la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo limesema linatoa msaada muhimu wa kibinadamu.

Katika taarifa siku ya Jumanne,  UNICEF imesema watu hao zaidi ya 40,000 wanajumuisha watoto 7,500 wa umri wa chini ya miaka 5 na wanawake wajawazito zaidi ya 1,500, na wamekimbia kutoka katika vijiji vilivyoko Uvira, Fizi na Mwenga wengine tangu mwezi Mei kutokana na mapigano ya kikabila ambayo yameathiri maisha ya maelfu ya watu.

Katika machafuko hayo UNICEF inakadiria kwamba vituo 10 vya afya viliporwa na kuharibiwa kiasi cha kutoweza kutumika huku vituo vingine 18 vikitelekezwa na wahudumu wa afya waliokimbia kulinda usalama wao.

Takriban shule 28 ziliporwa pia au kuharibiwa mwezi Desemba mwaka 2019 na hadi sasa hazijajengwa upya hivyo kuwaacha maelfu ya watoto bila mahala pa kusomea katika jimbo hilo.

UNICEF na wadau wake kwa sasa wanajikita kwa kazi na msaada wao katika eneo la Mikenge ambako watu 40,000 wamepata hifadhi katika maeneo ya porini ambako si mbali sana na maeneo walikotoka.

UNICEF imeonya kwamba hali ni mbaya sana kwa watu waliotawanywa katika milima ya Kivu Kusini wakihitaji haraka chakula, malazi, huduma za afya na msaada wa elimu, hivyo shirika hilo limetoa wito kwa wadau wa misaada ya kibinadamu kujitolea kusaidia haraka eneo hilo.

Ombi la fedha la UNICEF kwa ajili ya watoto wa DRC ni dola milioni 301 lakini hadi kufikia 15 Julai kwama huu ni dola milioni 27,000 tu zilizopatikana na zingine milioni 40 ni za mwaka jana hivyo kuacha pengo kubwa la dola milioni 219 sawa na asilimia 73 ya ombi lote.

342/